Sunday, March 17, 2013

Wananchi wataka UVIKIUTA idhibitiwe

WANANCHI wanaoishi maeneo ya Kivule mpakani mwa Wilaya ya Temeke na Ilala jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kudhibiti kikundi cha Umoja wa Vijana wa Kikristo Tanzania (UVIKIUTA), kuvunja nyumba zao, wakati mgogoro wao wa ardhi ukiwa bado mahakamani.

Mjumbe wa Shina namba 26 Mtaa wa Magole, Kata ya Kivule, Moris Kaombwe, alisema wananchi hivi sasa wanaishi kwa wasiwasi, kutokana na kikundi hicho kuvamia makazi yao nyakati za usiku na kuvunja nyumba zao, pamoja na kung’oa mboga katika bustani zao.

Kaombwe alisema, wanahusisha uvamizi huo na UVIKIUTA, kwani wana ugonvi wa kugombea mpaka na tayari kesi yao ipo mahakamani.

“Mgogoro wetu na UVIKIUTA upo mahakamani, hivyo tunashangazwa na hatua za kuvunjiwa nyumba zetu, na huo ni ukiukwaji mkubwa wa utawala wa sheria, ni vema sote tusubiri uamuzi wa mahakama.

“Lakini pia tunashangazwa na kikundi hicho, kudai eneo hili ni lao, wakati wao wako Temeke na sisi tuko Ilala, na katika zoezi la sensa mwaka huu, tulihesabiwa kama wananchi wa Ilala, sasa nani ni mkweli wa kufahamu mipaka hii, ni Serikali au UVIKIUTA?,” alisema na kuhoji Kaombwe.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia mgogoro huo, John Anania, alisema vijana wanaohusika na ubomoaji wa nyumba zao, wanakuwa wamevalia fulana nyekundu na suruali nyeusi, huku wakipeperusha bendera nyekundu na kuimba nyimbo mbalimbali.

Alisema hali hiyo, imezusha hofu miongoni mwa wananchi, ambapo Serikali isipoithibiti inaweza kusababisha mauaji na vita ya wenyewe kwa wenyewe katika eneo hilo.

“Kero yetu ni hawa majirani zetu UVIKIUTA, kwa kumtumia kiongozi wa Serikali hapa Dar es Salaam, wanatuma watu kubomoa nyumba za watu usiku ndani ya makazi, yanayopakana na makazi ya kikundi hicho.

“Hali hii ya uchokozi wa makusudi, ikiendelea inaweza kusababisha mauaji na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika eneo hili, hatutaki tufike huko, tunaiomba Serikali ichunguze kikundi hiki kinachotaka kuhatarisha amani kwa wananchi wake,” alisema Anania.

Naye, mlezi wa UVIKIUTA, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alipoulizwa alisema, amri ya kuvunjwa kwa nyumba zilizojengwa katika eneo la mgogoro, ilitolewa na Baraza la ardhi la Temeke, baada ya Wakili wake kulalamika kwamba, wavamizi wanaendelea na ujenzi katika eneo hilo lenye mgogoro.

Alisema mahakama, ndiyo iliyoidhinisha na kuteua dalali wa kuvunja nyumba hizo, hata hivyo alipoulizwa ni lini Mahakama hiyo, ilimteua dalali huyo, alisema aliteuliwa jana, muda ambao tayari nyumba hizo zilikwisha kubomolewa tangu wiki iliyopita.

Eneo la Kivule lenye mgogoro, lina ukubwa wa zaidi ya ekari 600, na wakazi zaidi ya 1,000 tayari wameweka makazi ndani ya eneo hilo, ambapo wanadai kuwa, eneo hilo ni mali yao na mpaka unaowatenganisha na UVIKIUTA ni barabara na si vinginevyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala (RPC), Marietha Komba, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hana taarifa, ameahidi kulishughulikia.

Vitendo vya jamii kujichukulia sheria mkononi, vimezidi kushamiri katika miaka ya hivi karibuni, ambapo baadhi yake vimesababisha maafa, yakiwemo mauaji ya watu wasio na hatia na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi.

No comments:

Post a Comment