Habari iliyotoka , 25 Oktoba 2012
WAKAZI zaidi ya 600 wanaoishi eneo la Kivule katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, wameazimia kumburuza mahakamani Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, kwa madai ya kutumia cheo chake vibaya na kutaka kuwanyang’anya ardhi wanayomiliki kihalali.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, wakazi hao walieleza kushangazwa na kitendo kilichofanywa na Rugimbana cha kufika katika eneo hilo lenye hekari zaidi ya 372 na kugawa vipeperushi vya kuwataka wakazi hao kuondoka kwa hiyari kabla ya kubomolewa nyumba zao.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi uliochaguliwa na wakazi hao, mjumbe wa kamati ya mgogoro huo, Barton Kigola, alisema mkuu huyo wa wilaya anatumia nguvu aliyonayo kutaka kuwaondoa katika eneo hilo, hivyo watamfikisha mahakamani ili waweze kutetea haki yao.
Kigola alisema mbali na kutumia nguvu aliyonayo, pia hukitumia kikundi cha Umoja wa Vijana wa Kikristo Tanzania (Uvikiuta) kuchukua ardhi hiyo.
“Hatuelewi kiongozi huyu anapata wapi idhini ya kutupokonya ardhi na hatuelewi kwanini anataka ardhi yote hii? Hata hivyo tunaiomba serikali wakichunguze kikundi hicho ambacho jina lake haliendani na matendo yake,” alisema.
Alisema eneo hilo lilikuwa mashamba ya wazawa ambapo mwaka 1974 baadhi ya wananchi waliondolewa katika operesheni vijiji na Rais wa awamu ya kwanza, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kigola alisema kutokana na wazawa kushindwa kulipwa fidia walilazimika kurudi katika maeneo yao na kuyaendeleza hadi sasa unapojitokeza mgogoro huo.
John Anania, alidai kabla ya kugawa vipeperushi hivyo baadhi ya vijana waliopo wa Uvikiuta walivamia eneo hilo Oktoba 17, mwaka huu majira ya saa 8:00 usiku na kubomoa nyumba zaidi ya saba zilizopo katika eneo hilo kwa madai ya kutumwa na kiongozi huyo.
Rugimbana alipotafutwa kuzungumzia madai hayo alikiri kuwa na uhalali wa eneo hilo na kumwomba mwandishi wa habari hizi kwenda ofisini kwake ili kuona nyaraka halali alizonazo za kumiliki eneo hilo.
“Naomba tuwasiliane kesho kwa kuwa kwa sasa nipo nje ya ofisi, ili nikuonyesha ushahidi nilionao. Kuhusu kutumia nguvu ya madaraka si kweli, kama wanaona hilo, basi wanifikishe katika vyombo vya kisheria, naamini huko ndiko kuliko na haki,” alisema Rugimbana.
No comments:
Post a Comment