!
Kijana akikoleza moto wa matairi wakati wa vurugu zilipokuwa zikiendelea katika Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya jana. |
Mamia ya polisi kutoka wilaya zinazouzunguka Mji wa Tunduma walimwagwa na walilazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji pia, kutuliza vurugu zilizodumu kwa zaidi ya saa nne.
Kutokana na vurugu hizo zilizoanza saa 4:30 asubuhi, wakazi wa mji huo walijifungia ndani kwa kuhofia usalama wa maisha yao, huku maduka na shughuli za biashara nazo zikifungwa.
Mwandishi wa gazeti la Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba katika vurugu hizo, watu zaidi ya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.
Habari zaidi zinasema barabara za mji huo zilifungwa, umeme ulizimika baada ya moto kulipuka kwenye moja ya nguzo za umeme. Pia mpaka wa Tanzania na Zambia ulifungwa kwa muda.
Magari ya abiria na yale ya usafirishaji yaliyokuwa yakitoka na kuelekea Zambia, Dar es Salaam, Sumbawanga na Mbeya Mjini pia yalikwama na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria. Msikiti ulivunjwa na watu wawili akiwamo askari polisi walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wahusika katika mgogoro wakiwamo viongozi wa dini na wachinjaji wa nyama.
No comments:
Post a Comment