Saturday, June 22, 2013

Wengi wameikosoa bajeti walalahoi kulia


Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa
Serikali jana iliwasilisha Bungeni mapendekezo yake kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14. Katika mapendekezo hayo, Serikali imepanga kutumia Sh18,248,983 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. 

Kwa tafsiri yoyote ile, bajeti hiyo inaonyesha bayana kwamba sio endelevu, kwani kati ya fedha hizo, Sh12,575 trilioni zitakuwa za matumizi ya kawaida wakati Sh5,674 trilioni tu ndizo zitatumika katika miradi ya maendeleo.

Matumizi hayo ya kawaida yanajumuisha shughuli zisizo za uzalishaji, zikiwamo mishahara ya watumishi wa Serikali, taasisi na wakala za Serikali, Mfuko Mkuu wa Serikali na kile kinachoitwa “Matumizi Mengineyo” ya Sh4.5 trilioni. 

Kwa maneno mengine, hii ni bajeti ya matumizi na sio ya maendeleo na haionyeshi dhamira ya Serikali ya kumkwamua mwananchi wa kawaida kutoka katika dimbwi la umaskini.
Matarajio makubwa ya Watanzania yalikuwa kuona bajeti ya kuwaletea unafuu katika maisha yao ya kila siku, bajeti yenye mwelekeo wa kuwapunguzia umaskini na kukuza hali ya kiuchumi kwa mtu mmojammoja, makundi mbalimbali na taifa kwa jumla. 

Watanzania wengi walitegemea bajeti hiyo ilenge katika kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu kupitia mfumo mpya uliowekwa na Serikali wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele inayotegemewa kuleta matokeo makubwa kwa haraka.
Matumaini hayo makubwa yalitokana na ukweli kwamba Bajeti hiyo iliyowasilishwa jana Bungeni ni ya kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa Maendeleo ya Miaka Mitano.

Mpango huo umeweka kipaumbele katika maeneo makuu sita ambayo ni Maji, Nishati, Elimu, Uchukuzi, Kilimo na Kuongeza Mapato.
Hata hivyo, Bajeti hiyo haionyeshi kuweka mkazo katika utekelezaji wa vipaumbele hivyo kwa vitendo wakati imetenga zaidi ya asilimia 60 kwa matumizi ya kawaida, huku miradi ya maendeleo kama barabara ikipewa fedha kidogo tu.

Hotuba ya Bajeti hiyo kwa kiasi kikubwa imejaa siasa na maelezo matamu ya jumlajumla tu. Uchambuzi wa haraka wa hotuba za Bajeti za miaka ya hivi karibuni unaonyesha kwamba Bajeti hiyo iliyosomwa Bungeni jana haitofautiani sana na hizo zilizopita isipokuwa katika maeneo machache tu.
Kwa mfano, Serikali inasema Bajeti ya mwaka 2013/14 ina shabaha na malengo ya uchumi manane, ikiwa ni pamoja na kuwa na akiba ya fedha za kigeni zitakazokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje. Hata hivyo, haisemi lolote kuhusu mkakati wa kupata fedha zaidi za kigeni kutokana na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zetu nje kwa lengo la kuweka ulinganifu wa kibiashara (Balance of trade). 

Hivyohivyo, Serikali inasema ina shabaha ya kupunguza mfumuko wa bei hadi digitali moja, lakini haisemi itatumia mkakati gani wakati mwaka uliopita mfumuko wa bei uliongezeka kwa asilimia 16 kutoka asilimia 12.7 mwaka 2011.
Mikakati mingi ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato haitekelezeki na ndio maana Bajeti hii inaendeleza utamaduni wa kupandisha kodi katika maeneo yaleyale tulioyazoea kama bia, sigara, vinywaji baridi, leseni za magari, mafuta na kadhalika. 

Kupanda kwa bei ya mafuta bila shaka kutapandisha bei za vyakula na gharama za huduma mbalimbali. Kichekesho kikubwa ni pale ambapo Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi imepunguzwa kwa asilimia moja tu kutoka asilimia 14 hadi 13.

No comments:

Post a Comment