Monday, June 17, 2013

IGP MWEMA AZUNGUMUZA KUHUSU BOMU ARUSHA

IGP MWEMA
DAR ES SALAAM, Tanzania
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema ameunda timu kwenda kufanya uchunguzi bomu lililolipuliwa mwishoni mwa mkutano wa kufunga kampeni Chadema, kwenye uwanja wa Soweto jijini Arusha jana na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 60 kujeruhuhiwa

Akizungumza leo, jijini Dar es Salaam , IGP Mwema amesema timu hiyo itaongozwa na Makamishina wawili kutoka Oparesheni na Idara ya Upelelezi Makao Makuu ambayo itakwenda haraka mkoani kwa ajili ya kuongeza nguvu katika Oparesheni na upelelezi.

Aliwataja watakaongoza timu hiyo kuwa ni Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo Paul Changonja na Kamishina Issaya Mngulu, kutoka idara ya Upelelezi wa makosa ya jinai na pia watashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Alisema Jeshi la polisi linalaani sana tukio hilo linaloashiria vitendo vya kigaidi ambalo limesababisha vifo na majeruhi kwa watu wasio na hatia pamoja na kujenga hofu miongoni mwa jamii.

"Napenda kuwahakikishia kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na Oparesheni kali pote nchini kuhakikisha linawasaka na kuwatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na kutenda uhalifu huo pia nawashukuru wananchi walianza kutupa ushirikiano wa kutupa taarifa za tukio hilo"

No comments:

Post a Comment